Habari

Chuo Chetu


Amiri Jeshi Mkuu alisema anajivunia kwa ndoto zake za kuanzishwa kwa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kutimia kwani sasa anapostaafu anaona fahari kutekeleza jambo aliloliahidi. “Nafurahi kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi huu, na ninaamini awamu ya pili ya kukamilisha majengo ya utoaji wa huduma na vifaa itaenda kwa kasi zaidi kwani hata mrithi wangu ajaye nitamuachia maelekezo pale nilipoishia”, alisema Mhe. Rais.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa Chuo hicho kwa Mhe. Rais, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Raphael Muhuga alisema ujenzi wa Chuo hicho ulianza rasmi Agosti 01, 2010 chini ya Jeshi la Kujenga Taifa kupitia Shirika lake la uzalishaji mali la SUMA JKT ambapo Wizara ya Ulinzi na JKT ilikuwa Mshauri Mwelekezi. “Hapo awali Chuo kilikuwa na jengo moja tu la utawala lililojengwa na Kampuni ya Tanzania Building Works kwa ufadhili wa Serikali ya Falme za Himarati (UAE) na kukabidhiwa rasmi Oktoba, 2007 jambo ambalo lilikwamisha chuo kuhamia hapo kutokana na kukosekana kwa madarasa, mabweni, bwalo, maktaba na jengo la kuzalishia vifaa vya kufundishia”, alisema Meja Jenerali Muhuga.
Aidha, Jenerali Muhuga aliongeza kuwa utekelezaji wa ujenzi huo umehusisha Brigedi ya 303 pamoja na mashirika matatu yaliyo chini ya Wizara ya Ulinzi na JKT ambayo ni SUMA JKT, Shirika la Nyumbu na Shirika la Mzinga. Alifafanua kuwa Brigedi imehusika na kuhakikisha kuwa barabara toka Tengeru hadi kuingia chuoni zimekamilika kwa kuzichonga na kuweka kifusi, ambapo SUMA JKT imehusika na ujenzi wa majengo kuanzia msingi hadi umaliziaji na uwekaji miundombinu ya maji na umeme. Shirika la Mzinga limehusika na utengenezaji wa barabara za ndani ya chuo na uwekaji wa samani, ‘grills’ za madirisha, milango ya aluminium na mandhari ya chuo pamoja na kujenga uzio kuzunguka chuo. NYUMBU walihusika na utengenezaji wa mifuniko na mfumo wa Maji Taka. Washiriki wote walitekeleza majukumu hayo chini ya uangalizi makini wa uongozi wa CSC.
“Kwa kutumia utaratibu huo wa matumizi ya taasisi za Jeshi katika utendaji kazi na upatikanaji wa vifaa kutoka maduka ya Jeshi, hadi kufikia hatua hii Jeshi limeweza kuokoa jumla ya Tshs 1,227,438,049.00/=. Takwimu hizi zinatokana na ulinganifu wa thamani ya mradi ilivyokuwa wakati wa kutolewa kwa zabuni (Ngome Tender Board) na gharama halisi hadi kukamilisha hatua hii ya kwanza”, alihitimisha Mkuu huyo wa JKT.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange alimshukuru Mhe. Rais kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho pamoja na kusaidia kutafuta msaada wa fedha kwa lengo la kukamilisha ujenzi huo ili kuhakikisha kada ya kati ya mafunzo ya ukamanda na unadhimu inahamia kwenye chuo chake cha kudumu. “Leo tunayo furaha kubwa kushuhudia uzinduzi rasmi wa chuo hiki katika eneo jipya la kudumu na hivyo kutimiza ndoto yako Mhe. Rais”, alisema Jenerali Mwamunyange.
Jenerali Mwamunyange alisema baada ya kutumia taasisi zake kukamilisha hatua hii ya kwanza ya ujenzi, dhamira ni kuwa uzoefu uliopatikana utautumika katika ujenzi wa majengo mapya ya shule ya mafunzo ya huduma Jeshini Pangawe, Morogoro ili nayo iwe na sura na mazingira ya kisasa yanayokidhi mafunzo yanayotolewa katika shule hiyo.
Akimkaribisha Mhe. Rais, Waziri wa Ulinzi na JKT Dkt. Hussein Mwinyi (Mb), alisema Wizara ya Ulinzi na JKT haitasahau juhudi binafsi za Mhe. Rais, michango ya hali na mali na maelekezo aliyoyatoa mara kwa mara katika kufanikisha ujenzi wa chuo hicho. Aidha, alizishukuru pia juhudi za dhati za Serikali nzima aliyoiongoza katika kufanikisha ndoto ya Serikali ya Awamu ya nne.
Akitoa historia ya Chuo cha Ukamanda na Unadhimu, Mkuu wa Chuo hicho Meja Jenerali Ezekiel Kyunga alisema kuwa Chuo hicho kilianzishwa Julai, 01, 1979 kufuatia uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Majeshi. Hivyo ilipofika Januari, 1980 kozi ya kwanza ilianza huko Fort Ikoma, Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara kwa wakati huo chuo kilijulikana kwa jina la Chuo cha Uongozi na Unadhimu – CHUU.
Jenerali Kyunga aliongeza kuwa mwaka 1989 Makao Makuu ya Jeshi yalipendekeza chuo hicho kihamisiwe Tanzania Military Academy (TMA) Monduli, mahali kilikoendesha kozi 23 katika kipindi cha miaka 26 hadi kilipohamia rasmi Duluti, Julai 2015 ambapo hivi sasa kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 60 kwa wakati mmoja. Hadi hivi sasa chuo kimefundisha jumla ya wanafunzi 889, kati yao Watanzania ni 674 na maafisa 215 toka nchi marafiki za Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, Waziri wa Ulinzi na JKT, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Daudi Felix Ntibenda, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na JKT Bw. Job Masima, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na JKT Bibi Mwitango Rose Shelukindo. Wengine ni Wakuu wa Kamandi, Matawi MMJ, Majenerali, Kamishna toka Wizarani na Maafisa wakuu wa ngazi mbalimbali, askari pamoja na wananchi walioalikwa.