Habari

Siku ya majeshi


JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza kuwa, kuanzia kesho Agosti 27 mwaka huu, litaanza maandalizi ya kuelekea tarehe Mosi Septemba mwaka huu, ambayo ni siku ya maadhimisho ya 52 ya majeshi, anaandika Zena Salehe.

Tarehe hiyo hiyo ndiyo siku ambayo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetengaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima ili kulaani kila wanachokiita udikteta unaofanywa na serikali ya awamu ya tano.

Tayari tangazo hilo la Chadema limepingwa vikali na Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani na Nsato Marijani, Kamishina wa Jeshi la Polisi, Operesheni na Mafunzo huku chama hicho kikiendelea kusisitiza azma yake.

Hata hivyo, Kanali Ngemela Lubinga, Msemaji wa JWTZ amesema kuwa, jeshi hilo limepanga kutumia siku hiyo kufanya maadhimisho hayo kwa kufanya usafi na upandaji miti katika kambi za jeshi na baadhi ya taasisi nchini.

Kanali Lubinga amewambia waandishi wa habari hii leo Jijini Dar es Salaam kuwa, “wananchi hawapaswi kuwa na hofu wala kutishika kipindi watakapoona wanajeshi katika maeneo ya karibu na makazi yao.

“Kesho tutaanza kufanya usafi kuanzia maeneo ya Kawe hadi karibu na kambi ya Lugalo, na wananchi watakapoona wanajeshi wengi mitaani wasiwe na hofu kwasababu hatuna nia mbaya na hivyo wasitufikilie vibaya,” amesema Lubinga.

Lubinga amesema mbali na jeshi kufanya usafi pia wanajeshi watajitolea damu salama katika hospitali za kambi za jeshi, “Sikukuu ya majeshi itaadhimishwa pamoja na wanajeshi kujitolea damu kwenye vituo maalumu vya kutolea damu salama mikoani na katika hospitali zetu za kanda,” amesema.
JWTZ pia imeahidi kuwa, madaktari wake watatoa huduma za kiafya bure ikiwemo upimaji wa virusi vya Ukimwi, kisukari na upimaji wa shinikizo la damu.