Administration Title | MKUU WA CHUO |
---|
WASIFU
Meja Jenerali Stephen Justice Mnkande ni Mkuu wa 18 wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu – Tanzania tangu Julai 13, 2023 hadi sasa. Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mwaka 1993 na kupata Kamisheni Mwaka 1994, Katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi – Monduli.
Meja Jenerali Stephen Mnkande ni Mhandisi wa Medani ambaye pia amehudhuria Kozi Ndogo ya Ukamanda na Unadhimu nchini Zimbabwe, Kozi za Ukamanda na Unadhimu nchini Uganda na Uingereza mtawalia, pamoja na Kozi ya Ulinzi wa Taifa nchini Tanzania.
Kwa upande wa Elimu ya Kiraia, Meja Jenerali Stephen Mnkande ni mhitimu wa Stashahada ya Ulinzi na Usalama ya Chuo Kikuu cha Zimbabwe, Shahada ya Uzamili ya Mambo ya Ulinzi ya “King’s College London” na Shahada ya Uzamili ya Usalama na Mambo ya Kimkakati ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi – Tanzania.
Akiwa jeshini, ametumia muda wake mwingi wa utumishi(miaka 21) kulitumika Jeshi kama Mkufunzi. Amekuwa Mkufunzi katika Shule ya Uhandisi wa Medani, Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi – Monduli, Kozi za Uongozi wa Platuni na Kombania, Chuo cha Ukamanda na Unadhimu - Tanzania na Chuo cha Ukamanda na Unadhimu - Zimbambwe katika Mpango wa Kubadilishana Wakufunzi Waelekezi. Aidha, amewahi kuwa Mkufunzi Mwelekezi Mwandamizi wa Jeshi la Nchi Kavu katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi – Tanzania.
Sambamba na nyadhifa hizo, Meja Jenerali Mnkande amewahi kuwa Kaimu Mkuu wa Tawi la Mipango na Maendeleo Jeshini, Mkurugenzi wa Mafundisho ya Kijeshi (Military Doctrine), Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi - Monduli na Msaidizi wa Mkuu wa Majeshi.
Pia, amewahi kuhudhuria Misheni mbalimbali za Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa akiwa Kamanda wa “Force Intervention Brigade (FIB) – MONUSCO” na “Military Observer (MILOB) – UNAMISIL - Sierra Leon”.
Vilevile kwa nyakati tofauti tangu kujiunga na JWTZ, Meja Jenerali Mnkande ametunukiwa nishani mbalimbali shahiki nje na ndani ya JWTZ hususan Utumishi wa Muda Mrefu, Utumishi Uliotukuka, Miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na Miaka 60 ya JWTZ.
Meja Jenerali Stephen Mnkande ni muumini mzuri wa kufanya mazoezi, kusoma vitabu na kusikiliza Mijadala ya Kimkakati.